Waumini Wapenzi wa Ahlul-Bayt (a.s.), viongozi wa dini, wanasiasa, wafanyabiashara na watu mashuhuri wameungana katika maandamano ya amani jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuhuisha kumbukumbu ya mauaji ya Karbala dhidi ya Imam Hussein (a.s.) na kusisitiza ujumbe wa haki, uadilifu na kupinga dhulma.

25 Juni 2026 - 18:31

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s.) –ABNA–, maelfu ya waumini na wananchi kutoka makundi mbalimbali ya kijamii wamefanya maandamano ya amani leo jijini Dar es Salaam, Tanzania, kwa ajili ya kuadhimisha kumbukumbu ya kuuawa shahidi kwa Sayyid wa Mashahidi, Imam Hussein (a.s), mjukuu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), katika ardhi ya Karbala.
 
Maandamano hayo yamewakutanisha waumini wa Ahlul-Bayt (a.s.l), viongozi wa kidini, wanasiasa, wafanyabiashara, watu maarufu pamoja na shakhsia mbalimbali, ambao walijumuika katika kuonyesha mshikamano wao na ujumbe wa Karbala wa kusimama upande wa haki, uadilifu na kupinga dhulma.
 
Washiriki wa maandamano walibeba mabango na bendera zenye ujumbe wa amani, haki na mapambano dhidi ya uonevu, wakisisitiza kwamba mapinduzi ya Imam Hussein (a.s) yanaendelea kuwa mwanga na chachu ya kupigania haki na utu wa mwanadamu katika zama zote.
 
Miongoni mwa wageni mashuhuri waliohudhuria maandamano hayo ni Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Tanzania, Mheshimiwa Himmat Panah, pamoja na Mwakilishi wa Jamiat Al-Mustafa (s) nchini Tanzania, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Dkt. Ali Taqavi.
 

Viongozi hao walisisitiza umuhimu wa kuendeleza ujumbe wa Karbala kwa kueneza maadili ya uadilifu, umoja, mapenzi kwa Ahlul-Bayt (a.s.) na kupinga aina zote za dhulma na uonevu katika jamii.
 
Washiriki wa maandamano hayo walieleza kuwa kumbukumbu ya Karbala si tukio la kihistoria pekee, bali ni shule ya milele inayowafundisha wanadamu kusimama imara mbele ya dhulma na kutetea haki, hata kwa gharama ya kujitolea nafsi zao.
 
Maandamano hayo ya amani yamehitimishwa kwa dua na maombolezo ya Imam Hussein (a.s.), huku waumini wakiahidi kuendelea kuhuisha ujumbe wa Karbala na kuurithisha kwa vizazi vijavyo ili maadili ya haki na uadilifu yaendelee kuishi katika jamii.

Your Comment

You are replying to: .
captcha